MAONO

MAONO

Na. Kelvin Kitaso

sehemu ya Kwanza

Pasipo maono watu hushindwa kujizuia” Mithali 29:18
Maono ni kama kesho ya mtu.Kesho ni siku ambayo hutarajiwa na haijaonekana bayana bado, na hakuna mwanadamu yeyote chini ya jua aijuaye kesho yake ipoje isipokuwa amejuzwa na Mungu ajuaye mambo yote kabla hayajatukia. Kesho ni siku ambayo ni matokeo ya kile kitu ambacho kimefanyika leo; kesho huandaliwa ndani ya leo, Mungu ndiye hutoa jawabu kama iwe kama vile ulivyoiandaa.
Kuna msemo wa kiingereza usemao, “Yesterday is history (jana ni historia), today is a gift (leo ni zawadi), tomorrow is a mystery (kesho ni siri iliyofichika)” hii inaonyesha kuwa katika maisha yote ya mwanadamu kuna siku tatu tu yaani jana, leo na kesho na mwanadamu anapaswa kuzitumia siku zote hizo kwa faida yake mwenyewe na kunufaisha jamii inayomzunguka pia.
Jana ni siku ambayo imepita na hukutengenezea uzoefu (CV) ambao waweza kuwa mzuri au mbaya, na kamwe hautoweza kurudi jana kuibadilisha jana yako ila unaweza kuitumia Leo kuifanya kesho isijekuwa kama jana. Jenga tabia njema ya kutojisifia kwa mazuri uliyofanya jana kwa kuwa kujisifia kutakufanya ujisahau kuwa unapaswa kusababisha mambo makubwa kutokea tena na tena kamwe usijaribu kujilaumu kwa vile ulivyoshindwa jana kwa kuwa itakufanya uwe muoga wa kujaribu kufanya mambo makubwa leo. Lakini mazuri ya jana yanaweza kutumika kama marejeo kuwa kama jana nilishinda basi na leo pia naweza kushinda kama ilivyokuwa kwa Daudi aliporejea kuua simba na dubu pale alipotaka kupambana na Goliathi.
Kesho ni mimba ambayo imetungwa leo na yapaswa kujifungua ni muhimu sana kuzingatia ili kuweza kujifungua mtoto aliye mzuri na hii inatokana na mimba hiyo imetungwaje na katika hali gani. Kujifungua mimba hii kunahitaji nguvu ya mbeba ujauzito na pia Mungu akusaidie kujifungua salama.
Maono huweza kuwa sawa na ahadi ambayo imetoka kwa Bwana kwa kuwa ahadi ni mambo yatarajiwayo na hayajaonekana bayana bado, ufananaji wake unatokana na kuwa ahadi ya Mungu huwa ni mambo ya kesho na ndiyo maana yanaitwa mambo yatarajiwayo na hayajaonekana bado, na yakichanganywa na hakika pamoja na bayana ambayo ndiyo imani hayabaki kuitwa maono au ahadi kwa kuwa tayari yametimia.
Kitu chochote unachokifanya leo kinaonesha kuwa kesho yako itakuwaje.
Ni lazima uione kesho yako ukiwa leo kwa kuwa kesho yako inategemea sana na wewe unaona nini ndani yako mwenyewe ukiwa leo, na si kuona tu, pia unakiri nini kwa kuwa kuna nguvu katika ukiri wa maneno, na si ukiri tu, bali ni nini ukifanyacho leo kinaweza kuitimiza kesho yako. Kitu ukionacho ndani yako, ukikiricho na hata kukifanya hugeuka kuwa tabia na kikiwa tabia mwishoni huja katika uhalisia wa utimilifu wake.
Kesho yako haitakuja kama muujiza yaani umeamka na kuiona tu inatimia, hapana ni mchakato mrefu ambao unakuhitaji kutia juhudi za kutosha ili iingie kwenye utimilifu wake. Kama haujaanza kuwaza kuwa kesho yako itakuja kuweje kamwe usijedhania kama kitakuja kutimia kwako kitu ambacho hujawahi kukiwaza hata siku moja, mtu anaweza kuhangaika na kitu ambacho amewahi kukiwaza hapo awali kuliko kile kitu ambacho hajawahi kuwaza kabisa.
Kijana mmoja alikuwa akisafiri kuelekea mahali asipopafahamu, baada ya kusafiri muda mrefu akakuta sehemu kuna njia panda na akamuona mzee mbele yake katika hilo eneo, akamuuliza Yule mzee nipite njia gani nifike sehemu ninayotaka kufika, Yule mzee akamuuliza mahali anapotaka kuelekea ili amuelekeze njia ya kupita; kijana akajibu kuwa hafahamu sehemu anayopaswa kwenda, Yule mzee akamwambia apite njia yoyote kati ya zile azionazo au hata arudi alipotoka pengine anaweza kufika mahali anapotaka kufika. Mfano huu ni sawa na mtu asiye na maono katika maisha yake ni lazima awe mtu anayeshindwa kujizuia na hana muelekeo maalum.
Lazima uione ndani yako kwanza. Mwanadamu huwa vile anavyowaza ndani yake kwa kuwa lile wazo humpa hamasa ya kufanya kazi ili litokee na wazo pia la ndani yake huweza kumfanya kukata tamaa ya kufika mbali. Mtu mmoja akasema kuwaza ni kuwaza tu kama umewaza mambo makubwa au madogo ni bora ukawaza vitu vikubwa labda waweza kuwa mtu mkubwa. Lakini kuwaza tu pasipo kuchukua hatua hakufai. 
Mithali 23:7 “7 Maana aonavyo nafsini mwake, ndivyo alivyo.” Yaani ukitangulia tu kuona kuwa wewe ni maskini mkubwa ni lazima uwe, ni lazima ujifunze kuona vyema. Watu wakubwa duniani kabla ya kuwa vile walivyo, walitangulia kuona ukubwa ndani yao kwanza na kisha wakaanza kufanya kazi kwa kuwa ile picha waliyoiona ndani yao huwatesa kuifikia.
Katika biblia neno ‘unaona nini?’ limeonekana mara saba na siku za wiki zipo saba, ina maana ya kusema kila asubuhi BWANA huweza kukuuliza ‘unaona nini?’ mpaka zikaisha siku saba za wiki na itakapoanza jumatatu ataanza na unaona nini? tena mpaka Ijumaa huku akiunganisha na neno usiogope kwa kila siku uionayo katika uwepo wako duniani.
Kofi Anan ambaye ni katibu mkuu wa zamani wa umoja wa mataifa baada ya kuingia UN katika nafasi ya kawaida tu akamwandikia mama yake ujumbe na kumtaarifu kuwa siku moja ni lazima aje kuwa katibu wa umoja wa mataifa. Alivyoona ndivyo ilikuja kutokea na kule kuona kwake kulimlazimu kutotulia na kuwa na juhudi kubwa sana ili baadae aje kuwa katibu mkuu wa umoja wa mataifa.
Kama kuna picha tayari unaiona ndani yako ya jinsi vile unavyopaswa kuwa ni muhimu sana kuzingatia kuwa picha ile ni nguvu ya kukufanya upigane hata kuitimiza; ila mbaya zaidi ni kwa mtu asiye na maono kwa kuwa hana picha ndani yake ni vigumu kwa yeye kufanya kitu cha msingi.
Maandiko yanasema katika Mithali 29:18 kuwa “18 Pasipo maono, watu huacha kujizuia”, tafsiri ya asili ya kiebrania maono imetafsiriwa kama ‘hazon’ ambayo humaanisha mafunuo ya neno la Mungu, na huendelea kwa kumaanisha kuwa pasipo neno la Mungu kufunuliwa kwa watu ni lazima watu waende katika njia ya upotevuni. Mahali popote ambapo neno la Mungu halijafunuliwa ni lazima watu waangamie na kuendelea katika njia zao wenyewe kwa kuwa bado huwa kwenye mabano ya wafanye kipi na kuacha kipi.
Kwa kuangalia maono pia mtu yeyote ambaye hajafunuliwa ni maono gani alionayo ni kazi sana kuwa katika njia sahihi. Jamii inayotuzunguka watu wengi hukosa maono na ndiyo maana huishia kufanya vitu vya ajabu sana. Maono ni ile picha ya ndani aionayo mtu kwa habari ya kesho yake na kama mtu haoni picha yoyote ndani yake ni vigumu kufanya vitu vya msingi vya kimaendeleo.
Mtu mwenye maono hata kama anaonekana maskini kwa wakati huo ni mtu wa tofauti kwa kuwa maono ni muongozo wa utendaji kazi wa mtu huyo na ni lazima afanye mambo ambayo yanapelekea utimilifu wa maono hayo na huishi maisha ya kujizuia katika mambo yoyote ambayo hayamsaidii kufikia mwisho wake. Mtu mwenye maono hawezi kutulia hata maono yake yawe yametimia.
Maono hutoa muongozo wa jinsi mtu apasavyo kuwa na hata jamii ya kushirikiana nayo.
Nikiwa sehemu fulani nahudumu baada ya huduma nikamuuliza kijana mmoja, je! Unataka kuja kuwa nani? yule kijana akaniambia nataka kuja kuwa dereva na alikuwa anasoma, na nilipomuuliza kwa nini anataka kuja kuwa dereva alieleza kuwa, ni kwa sababu wazazi wake hawana uwezo wa kumuendeleza kimasomo, nilitafakari kuwa mtu huyu anataka kuja kuwa dereva kwa sababu ya hali ngumu ya kiuchumi, ni vizuri ila katika mazungumzo nikagundua kuwa amekata tamaa ya kufanikiwa zaidi kwa sababu ya hali yake ila mwenye maono hata kama ana hali ngumu kamwe hataacha kuukiri ushindi wake kuwa pamoja na ugumu uliopo ninaweza nikafika pale ninapokusudia na hata kama nitachelewa kulingana na vikwazo vya hali niliyonayo sasa ila nitahakikisha nimefika.
Pamoja na kuwa mfanya kazi wa ndani kwa Potifa na kisha kupelekwa gerezani na kuwa mfungwa, bado Yusufu aliendelea kuitazama na kuikiri ndoto yake ya kuja kuwa mtu mkubwa, mazingira mabaya na ya kukatisha tamaa hayakumfanya Yusufu akate tamaa na kubadilisha aina ya ndoto. Ni ukweli sana kuwa ugumu wa maisha ni sababu kuu sana ya kusababisha watu kuyaacha maono yao ya uhalisia na kuingia katika mengine ambayo si maono yao.

Mtu asiye na maono ni lazima mambo yake yawe ovyo ovyo kwa kuwa hakuna mwongozo sahihi unaoweza kumzuia asifanye yale ambayo anataka kufanya. Maono ni muongozo kwa mtu mwenye nayo katika mambo yote na humuongoza kuwa sehemu sahihi kwa wakati sahihi na kuwa na watu sahihi. Na ni nadra sana kumkuta mtu mwenye maono anafanya mambo ambayo hayawezi kumsaidia kufikia utimilifu wa maono yake.
 Ni muhimu sana kwa mtu kuiona kesho yake ndani yake na aione katika uzuri ndipo anaweza kutumia muda wake vizuri kutimiza yale ayaonayo. Kuona ni jambo jema sana ila mtu anaweza kuogopa kuwaza mambo makubwa na hii hutokana na mtu kujidharau na kuona kuwa ana uwezo mdogo sana ndani yake, hili ni tatizo la kiimani, kutojitambua na kujidharau; ni lazima utoke kwenye eneo hili la kukosa kujiamini na uanze kuona kuwa unaweza.
Maono makubwa, huleta taabu kubwa, (The greater the revelation, the greater the tribulation)
Wakati fulani nikiwa na rafiki yangu Christina akanena na kuniambia kwamba “the greater the revelation, the greater the tribulation,” akimaanisha kuwa (maono makubwa huambatana na taabu kubwa). Ukifuatilia kwenye biblia utaona kuwa watu wote waliobeba maono makubwa ndio watu waliopata taabu kubwa hata utimilifu wa maono yao. Usikate tamaa unapoona majaribu yamekuwa ni makubwa sana kwa upande wako, kaa utulie huku ukitafakari kuwa ni uzito wa maono uliyonayo ndiyo sababu kuu ya kuteseka kwako.
Mfano ni Mtume Yohana aliyepata maono ya kitabu cha ufunuo akiwa katikati ya mateso makubwa na kuwekwa katika kisiwa cha Patmo na Mtume Paulo ambaye alipata mateso makubwa kulingana na ukubwa wa maono aliyokuwa amebeba.

itaendelea sehemu inayofuata...................
 




Comments