SOMO: VITU VITAKAVYO KUSAIDIA UISHI KWA KUUKOMBOA WAKATI
MWL. KELVIN KITASO ....... 0713804078
1. Kuishi kwa malengo.
Ukiwa na malengo katika maisha yako ni lazima
utumiaji wa muda utakuwa ni tofauti na wengine wanavoweza kutumia. Lazima uwe
na malengo kwa kufahamu unataka nini katika maisha. Watu wote wanaofanikiwa huwa
ni watu ambao wanamalengo, yaani wanafahamu wanahitaji nini? Ukiwa haujui
unachokihitaji katika maisha kila kitu utakachokifanya katika maisha yako bado
utakiona kipo sawa.
Malengo ndiyo yatakufanya usitulie, ndiyo
yatakayoongoza maamuzi yako na ndiyo yatakayokuwa kiongozi katika kutumia muda
wako.
2.
Orodhesha mambo ya kufanya mara kwa
mara kabla haujaanza kufanya.
Ni vibaya kuamka asubuhi hujui unafanya nini, au
unaenda wapi au unapaswa kukamilisha nini kwa siku hiyo. Ukiwa unaishi katika
mfumo wa maisha kama hayo chochote kwako kikitokea utaona ni sawa,
ukishawishiwa kwenda popote bado utaona ni sawa na utakubali kwenda.
Ni vyema zaidi kila siku ikawa na ratiba maalumu
ya nini unapaswa kufanya kwa siku hiyo na wapi unapaswa kuelekea katika siku
hiyo. Paulo alipokuwa anawaandikia waraka Wathesalonike aliwaonya wawe watu
wanaoenenda kwa utaratibu, kuenenda kwa utaratibu ni kuwa watu ambao wanajua
nini wanapaswa kukifanya na kwa muda gani na kisha kukifanya. Usipokuwa na
maarifa ya kufahamu nini unapaswa kufanya kwa siku hiyo si rahisi ukafanikiwa.
Kila siku inapoanza lazima uwe unajua kuwa kwa
leo napaswa kukamilisha jambo Fulani, na hakikisha kuwa linakamilika. Usikubali
kuimaliza siku yako bila kukamilisha lile ambalo ulipaswa kulikamilisha.
Rafiki yangu Christina huwa anapenda kunisisitiza
kuwa hatuendi kulala kwa kuwa usiku umeingia ila tunalala kwa kuwa tuliyopaswa
kuyakamilisha kwa siku ya leo tumeyakamilisha kwa ukamilifu, na kisha
kumshukuru Mungu atupaye nguvu ya kukamilisha. Na siku ikianza tu bila kumuomba
nguvu za kuikamilisha mipango huwa ni siku nzito sana, siku moja alinipigia
simu akihudhunika kuwa siku yake imekuwa mbaya sana, nikamuuliza kwa nini?
Akanieleza kuwa aliondoka nyumbani bila ya kumuomba Mungu amtangulie ndiyo
maana ameteseka sana.
Unapolala mshukuru Mungu kwa kukupa nguvu ya kufanikisha yale
uliyokuwa nayo kwa hiyo siku, na unapoamka muombe Mungu akupe nguvu tena ya
kutekeleza yale uliyonayo kwa siku ya leo.
Nimejifunza kwa mtumishi wa Mungu Nabii T.B
Joshua anayesema kabla ya mambo yote mkabidhi Mungu mambo yako kwa kumwambia,
Oh! Lord Jesus, take more of me, and give me more of you” yaani, “Bwana Yesu, chukua yaliyo yangu na
unipe yaliyo yako”
Watu wanaofanikiwa ni watu ambao wanaenenda kwa
utaratibu na wanaratiba kila siku za kufanya na ndiyo maana ukihitaji kuonana
na watu waliofanikiwa si rahisi ukakurupuka tu na ukafika ofisini kwao na
ukawakuta, kwa kuwa kila dakika yao imepangiliwa, ila watu ambao hawajui kwenda
kwa utaratibu ni rahisi sana kupatikana kila wakati kwa kuwa wanamuda na dakika
za kutosha na hata wakiupoteza hawapungukiwi na kitu.
3.
Ishi maisha ya vipaumbele.
Kuwa na vipaumbele katika vile vingi ulivyonavyo
kutakusaidia sana kutumia muda wako vizuri na kukuzalia matunda mazuri. Uwe na
concentration katika vipaumbele vyako vya hiyo siku. Kama umesema kuwa naanza
kusoma kitabu Fulani, hakikisha unasoma mpaka unakimaliza ndipo upate nguvu ya
kuendelea na mengine.
Watu wengi wanafanya vitu lakini hawana
concentration katika yale wanayoyafanya na ndio maana huwa hawamalizi, unakuta
mtu anaanza kitu Fulani hakimalizi na anaishia katikati.
4.
Jiwekee muda wa kukamilisha
(deadline).
Ili uweze kuwa mtumiaji mzuri wa muda usianze tu
kitu halafu ukawa unafanya fanya tu. Jiwekee muda wa kumaliza hiko kitu
unachokifanya, deadline itakuwa ni nguvu inayokusukuma kufanya kile
ulichonacho.
Wakati Mungu anafanya uumbaji alijiwekea muda
kuwa mpaka kufikia siku 7 ni lazima uumbaji uwe umekamilika na ndivyo
alivyofanya, kila siku akaipa majukumu yake ili tu kuhakikisha anakamilisha
kile alichoadhimia kukifanya, ila pia aliweka vipaumbele katika vile
alivyofanya, alikusudia kumuumba mwanadamu ila hakumuumba siku ya kwanza,
utagundua hakumuumba siku ya kwanza kwa kuwa hakikuwa kipaumbele chake cha
kwanza katika uumbaji wake lakini pia kama angemuumba siku ya kwanza angekuja
kufanya nini kama angekuta kila kitu bado hakijaumbwa na udongo wa kumfinyangia
angeutoa wapi?. Mungu akaona huyu awe wa mwisho ili akute kila kitu.
Tengeneza udongo kwanza kabla hujaanza kuumba
Utagundua kipaumbele cha Mungu ilikuwa ni kuanza
na mengine kwanza ikiwemo udongo ili kazi ya kuumba isije kuwa ngumu. Na masaa
24 ya mwisho tayari alikuwa na udongo hivyo akayatumia vizuri sana masaa hayo
kwa ustadi mkubwa kumtengeneza mwanadamu.
Unapoanza ni vyema ukaanza na kutengeneza udongo
kwanza utakaokusaidia kutengeneza kile unachokitaka, usianze kuumba mtu wako
kabla hujawa na udongo, na ukikosea hapo kazi ya masaa 24 utaifanya kwa miaka
24 na bado haitakamilika.
Hata wewe unavyofanya mipango ya maisha yako ni
lazima uweke orodha ya vitu muhimu, kisha ujiwekee muda wa kuvikamilisha, kisha
uchague vipi vya kuanza navyo na uanze kuvifanyia kazi. Hata kama ni malengo
yako usifanye kila kitu kwa huo wakati, fanya vyenye kipaumbele tu.
5.
Anza kufanya sasa.
Usiseme kuwa nitafanya, anza kufanya sasa. Wengi
wanamipango mizuri na haitimii kwa kuwa ni wavivu wa kutendea kazi na mara
nyingi husema nitafanya. Katika kuukomboa wakati, hakikisha unaanza sasa na
uanzie pale ulipo.
Tafakari kama Mungu angesema “tutaumba” nafikiri
mpaka sasa angekuwa anaahirisha ikimjia ratiba nyingine angekuwa anaahirisha
tu, ila yeye alisema “natumfanye” maanaake tuanze kufanya sasa. Hauna muda wa
kupoteza kuwa nasubiri nipate hela ndipo nianze.
Anza hapo hapo ulipo tengeneza jitihada za
kutosha ndipo mafanikio ya kweli yanatokea kwa namna hiyo. Kumbuka kuwa huna
muda wa kusubiri kuanza hilo unalotaka kulianza. Muda mzuri wa kuanza ni sasa.
Watu wanaofanikiwa ni watu wanaothubutu kuanza
kufanya bila kusubiri chochote ila watu wengi wasio fanikiwa hawafanikiwi kwa
sababu huwa hawaanzi kufanya, wanapenda kusubiri subiri. Utawasikia wanasema
nikipata milioni 1 nitaanza biashara, ila wanaofanikiwa wakipata hata 10,000/=
huwa wanaanza bila kusubiri.
6.
Achana na kila kinachokupotezea muda.
Inaweza ikawa ni watu unaoshirikiana, mitandao,
video unazoangalia. Kuwa makini kuachana navyo vyote maana vinaweza kukuharibia
malengo uliyonayo.
Watu wengi wanaweza kuwa ni wapoteza muda tu, na
hakuna vitu vya msingi mnavyoweza kuvifanya kuwa na future iliyonjema. Watu
kama hao achana nao. Unaweza ona mtu anapiga simu muda wa kazi na anakuambia
nimekumiss nilikuwa nataka kukusalimia. Ni nzuri inahimarisha ushirikiano ila
haina umuhimu kwa kuwa ni wakati wa kutekeleza majukumu mengine. Mtu akikupigia
simu wakati wa kutekeleza majukumu yako si lazima kuipokea simu yake kwa kuwa
inaweza kuambatana na taarifa ambazo zinaweza kukutoa katika majukumu
unayoyafanya.
Kama kuchati kunakupotezea muda achana nako ili
utimize mambo ya msingi. Ukweli ni kwamba kuchati hakuna hatima nzuri ya maisha
yako, kuwa makini kila wakati na namna unavyofanya, kuna watu wapo makundi ya
kuchati mengi sana na mengi yao hayana hata faida kwao ila wamo tu, tafsiri
yake hawa ni aina ya watu ambao hawajui wapi wanaelekea. Watu wanaojielewa
huwezi kuwakuta wanachati chati tu bila mpangilio au wapo kwenye makundi mengi
yasiyo na maana na hata ukiwakuta kwenye makundi ujue kuna mambo ya msingi
wanafanya au wanayatumia kwa faida ya kufikia malengo yao.
Ili kubadilika unahitaji kubadilika.
7.
Fanya tathmini juu ya malengo
unayojiwekea
Katika malengo uliyojiwekea katika siku hiyo
kabla hujalala jipe muda wa kujitathimini ni mangapi umeyatimiza na mangapi
haujayatimiza, nay ale ambayo hujayatimiza ni nini kimekusababisha usitimize,
ili kesho uhakikishe unakuwa makini kutorudia kosa lile lile.
Mfano mzuri ni Mungu mwenyewe kila siku alipokuwa
akimaliza majukumu yake alifanya tathmini ya kazi yake na akahitimisha kwa
kusema kila kitu kilienda vyema. Hakuanza shughuli za siku ya pili kabla ya
kufanya tathmini ya siku ya inayoisha.
WAWEZA AGIZA NAKALA ZA KITABU CHA MAMBO 20 YATAKAYOKUFANYA UFURAHIE MAISHA YAKO KUPITIA NAMBA 0713 804 078.
Comments
Post a Comment