MAONO
NA MWL. KELVIN KITASO
Sehemu ya pili (2)
Kwani wao
waweze wana nini na sisi tushindwe tuna nini?
Katika jamii ya waswahili huu ni msemo ambao umekuwa
ukitumika sana na ni miongoni mwa misemo ambayo imejipatia umaarufu mkubwa
sana. Ni kweli kuwa wapo watu wafanyao mambo makubwa na yakatokea lakini
wengine hushindwa kufanya mambo hayo. Wafanikiwao nao ni watu kama walivyo watu
wengine ila utofauti mkubwa hujengwa katika namna ya kufikiria na pia katika
namna ya kufanya mambo. Watu wote walio juu ukifuatilia historia zao utakuta
walikuwa ni watu wa kawaida sana, ila ndani yao waliweka nia na kuamua
kupambana kufikia hatua kubwa na za juu, na watu wa namna hii hata walipopata
mafanikio madogo hawakubweteka na kujisahau bali walizidi kusonga mbele kupata
mafanikio makubwa zaidi. Kama wao wamejaribu wakaweza kwa kutia nia na wewe
ukitia nia kwa lolote ufanyalo ni lazima utaweza tu.
Mfumo wa kuzaa kwa viumbe
Nikiwa na rafiki yangu tunazungumza na kutiana moyo kwa
habari ya safari tuliyonayo akazungumza neno jema sana kuhusu maono kwa
kufananisha na wanyama, kuwa wanyama wadogo hubeba mimba na kujifungua kwa muda
mfupi; wengine hubeba kwa miezi mitatu (3), wengine ni sita (6) na wengine ni
tisa (9), tofauti huwa kwa wanyama wakubwa kama tembo wao hubeba mimba yao kwa
muda mrefu sana ukilinganisha na wanyama wengine, hii ni kwa sababu ya ile
asili yao ya ukubwa ambayo Mungu amewawekea.
Kwa
kuutazama mfano huu ndivyo ilivyo kwa sisi wanadamu ya kuwa maono makubwa
huweza chukua muda mrefu sana kabla ya kutoka na mtu mwenye maono makubwa
huchukua muda mrefu pia kufikia utimilifu wa maono yale. Usiumie kwa nini
wengine wanatoka upesi na wewe unapambana ila bado; fahamu aina ya maono
uliyobeba pengine ni mazito kama mimba ya tembo na kama ndivyo yaweza kaa muda
mrefu hata utimilifu wake ila yatatokea tu kwa kuwa maono ni kama mimba.
Mbali na
wanyama pia kwa mimea kuna neno jema la kujifunza kwa kuwa kuna miti ambayo
hupandwa na kukua kwa muda mfupi na huvunwa ndani ya muda mfupi huo, ila kuna
mimea ambayo hukaa sana na huchukua miaka mingi sana hata kufikia utimilifu
wake, kwa kuchukulia mifano kama mnazi, hata mbuyu hukaa kwa kitambo kirefu
sana hata kuja kutoa matunda yake.
Hii
inaonyesha kuna utofauti mkubwa sana wa utimilifu wa maono ya mtu mmoja mpaka
mwingine, kuna wengine ambao hushuhudia utimilifu wa maono yao kwa haraka sana
ukilinganisha na wengine. Muda wa kuchelewa kwa maono ya mtu Ibilisi huutumia
sana kuwa shawishi watu kuona kuwa Mungu hayupo pamoja nao, na huweza kusema,
mbona hujabarikiwa kama fulani na fulani na wewe unamtumikia Mungu kama wao, au
ulimaliza nao chuoni au shuleni au ni marafiki wa karibu ukishiriki nao mengi
sana ila wao wamekupita kufanikiwa kwa kuwa Mungu hajali mambo yako na
huwapenda wenzako kuliko wewe; wewe usikatishwe tamaa na sauti ya kinyonge
namna hiyo songa mbele maana utimilifu wako unakuja na ufanikiwaji wa mtu mmoja
na mwingine huwa tofauti na kwa nyakati tofauti tofauti.
Mtu mwenye
maono hawezi kutulia hata atimize maono aliyonayo na hata akishindwa mara moja
huinuka na kujitia nguvu na kutokata tamaa na ni maono ambayo humsaidia mtu
kuishi kwa kuukomboa wakati, kuweka vipaumbele vya maisha ambavyo vitampelekea
kufikia utimilifu wa maono hayo, kuchagua watu sahihi wa kuambatana nao ambao
watamsaidia kufikia hatima ya maisha yake.
Kutokuwa na vipaumbele katika maisha.
Kukosa
maono kunapelekea mtu kushindwa kujizuia na huku kushindwa kujizuia ndiko
kunamaanisha kutokuwa na vipaumbele. Mtu yeyote mwenye maono ni lazima atakuwa
na vipaumbele vya msingi katika maisha yake na vipaumbele hivyo humsababisha
kufikia utimilifu wa maono aliyonayo.
Vipaumbele
ni vitu ambavyo hupewa umuhimu wa hali ya juu na hupewa umakini mkubwa zaidi ya
vitu vingine vyote. Na vitu hivi huweza kuchukua muda mwingi wa mtu kuliko vitu
vingine vyote na mtu huwa makini sana kutoruhusu vitu vingine ambavyo
vitaharibu utaratibu uliopo. Vipaumbele husababisha utimilifu wa maono
aliyonayo mtu na humfanya mtu kuzingatia kuwa sehemu sahihi, wakati sahihi na
watu sahihi.
Kwa mfano
mwanafunzi awapo shuleni ni lazima awe na vipaumbele vya msingi kama kumtumikia
Mungu kama balozi wa Yesu katika eneo asomalo na kusoma kwa bidii zote, kwa
kuwa ni jukumu la msingi pia lililompa kuwepo mahali hapo. Na si kwa wanafunzi
tu bali hata aliyepo kazini ni lazima awe na vipaumbele vya msingi
vitakavyomsababishia kufanikiwa katika kufikia hatima yake iliyo njema.
Asiye na
vipaumbele hufanya mambo yake pasipo mpangilio na huwa ni mtu asiye na misimamo
juu ya yale ayafanyayo na hukosa kujitoa kikamilifu katika mambo ayafanyayo.
Katika
vipaumbele ni vyema kuzingatia kuwa kila jambo katika ulimwengu huu lina majira
yake, na nyakati zake na utambuzi huu utamfanya mtu kufanya kitu sahihi katika
wakati sahihi na kuepuka kufanya jambo ambalo lipo nje ya wakati.
Mambo ya
msingi katika kufanikisha vipaumbele vyako.
- Chagua marafiki sahihi.
- Kuwa mahali sahihi, sehemu sahihi na ukifanya jambo sahihi.
- Kila jambo ulifanyalo zingatia wakati kwa kuwa kila jambo lina wakati wake na majira yake/ukomboe wakati.
- Ishi kwa malengo, timiza malengo yako.
- Usiishi maisha ya kuigiza, ishi maisha yako.
- Tumia vyema fedha uzipatazo hata kuweka akiba ya kukusaidia baadae.
- Kuwa hodari na moyo wa ushujaa/ usiogope kwa kuwa yapo mengi yaogopeshayo ila sababu ya kutoogopa ni kuu zaidi ya hayo yote.
- Mwamini Mungu.
- Jiamini wewe mwenyewe kuwa unaweza.
Mungu Anaona Ambayo Wengine hawaoni juu yako.
Ikiwa Mungu aliona taifa kubwa ndani ya Yakobo mchunga
mifugo wa Labani, akaona Waziri Mkuu ndani ya Yusufu mfanya kazi wa ndani na
mfungwa kule Misri, akaona mkombozi wa Israeli kwa Musa mchunga mifugo kule
Midiani kwa Kuhani Yethro, Akamwona Mwamuzi wa Israeli Gideoni yeye Ambaye
alikuwa dhaifu na kutoka katika familia ya hali ya chini sana, Akamwona Yefta
aliyekataliwa na ndugu zake na kumfanya kuwa mwamuzi wa wana wa Israeli, Akaona
Mfalme wa Israeli ndani ya Daudi Mchunga mifugo na hakutazamiwa hata na baba
yake, Akaona Mwokozi wa ulimwengu na Mfalme wa mataifa katika Zizi la Ng’ombe
(Yesu). Leo hauzuiwi na hali uliyonayo wewe kukufanya mtu mkubwa, usiache
kumtumaini ni lazima atafanya alichokusudia kwako.
Comments
Post a Comment