JESHI LA PEKEE LINALOWAUA ASKARI WAKE WALIOJERUHIWA NA KANISA LA YESU KRISTO
Mwl: CARLOS RICKY WILSON KIRIMBAI



Mpendwa msomaji wangu unaweza ukawa unakosea sana katika namna unavyoshughulika na mambo mbalimbali unayokutana nayo maishani na ukajiona upo sawa tu.
Moja ya mahali ambapo unakuta badala ya kumsaidia mtu aliyeharibu au kukosea tunammalizia kabisa ni Kanisani.
Ni ajabu sana umkute mtu amepata shida au ajali na badala ya kumsaidia kwa kumkimbiza hospitalini au kumpa huduma ya kwanza, wewe ukaamua kumalizia ili umwue kabisa.
Inakuwa mbaya sana pale unapoamini kabisa kuwa unachofanya ni ibada kwa Mungu.
Kanisani hatuui watu kwa mapanga, wala visu, mikuki wala mishale, hatuwaui kwa risasi bali kwa maneno.
Tunaua sifa zao na muonekano wao katika jamii (character assasination).
Tunanukuu maandiko ya kuhalalisha tukifanyacho huku tukiyasahau au kuyapuuzia kabisa maandiko yanayoagiza vinginevyo.
Ndugu zangu, mtu akighafilika katika kosa lo lote, ninyi mlio wa Roho mrejezeni upya mtu kama huyo kwa roho ya upole, ukijiangalia nafsi yako usije ukajaribiwa wewe mwenyewe. (GAL. 6:1 SUV).
Hapa ni wazi kabisa kuwa mmoja wetu akighafilika katika neno lolote walio wa Roho (sio tu kila mtu) wamrejeshe huyu mtu kwa roho ya upole (sio maneno makali ya kushambulia facebook na insta na kwenye mitandao ya jamii) na akituonya tuangalie sana nafsi zetu tusije kujaribiwa sisi wenyewe.
Kosa la mwingine linaweza kukupelekea ukosee kuliko huyo ambaye umebaki kujadili kosa lake na kumwita kila aina ya majina yasiyo na staha au kiasi.
Tumeambiwa tujitahidi katika upendano wa ndugu na upendano wa ndugu unafunika kosa na sio kulianika.
Kuchukiana huondokesha fitina; Bali kupendana husitiri makosa yote. (MIT. 10:12 SUV).
Sio wivu wa nyumba ya Mungu ndo unatusukuma kuanikana hadharani bali ni chuki tuliyo nayo moja kwa mwingine ndo inatupelekea kuanikana hadharani na wivu tuliyo nao mmoja kwa mwingine.
Haiwezekani kuanguka kwa mmoja wetu badala ya kuwa msiba kwetu ndo inakuwa sherehe kwetu.
Tumekuwa kuwa kama ndege wala mizogo (vultures).
Tumekuwa kama fisi wala mizoga. Kwanini tunafurahia kula mizoga ya wengine?
Kwanini tunajilisha na makosa ya watu wengine? Au labda inatufanya kwa muda tuyasahau ya kwetu wenyewe?
Upendo siku zote utatusukuma kusitiri makosa ya wengine.
Zaidi ya yote iweni na juhudi nyingi katika kupendana; kwa sababu upendano husitiri wingi wa dhambi. (1 PET. 4:8 SUV).
Juhudi katika kupendana sisi kwa sisi kutatupelekea tuwe wepesi zaidi kusitiririana kuliko kuanikana.
Sasa mmoja anaweza kusema ina maana tuunyamazie upuuzi ambao unafanyika kati yetu?
La hasha.
Lakini sio kwa kuanikana na kudhalilishana hadharani.
Mungu katuwekea utaratibu mzuri wa kushughulika na mambo yetu.
Tukumbuke kuwa kanisa ni la Mungu hata hivyo na sio letu na Yeye Ndiye anaweka utaratibu wa kushughulika na vitu miongoni mwetu.
Na ameshasema walio wa Roho kati yetu wamrejeshe sio kumtenga, kumsema, kumsengenya na kumshambulia huyo mtu.
Ameshasema tusitiri wingi wa makosa na sio kuanika.
Ameshasema tusitiriane.
Maandiko yanasema:
Usiende huko na huko katikati ya watu wako, kama mchongezi; wala usisimame kinyume cha damu ya jirani yako; mimi ndimi BWANA. Usimchukie ndugu yako moyoni mwako; ni lazima kumkemea jirani yako, wala usichukue dhambi kwa ajili yake. Usifanye kisasi, wala kuwa na kinyongo juu ya wana wa watu wako; bali umpende jirani yako kama nafsi yako; Mimi ndimi BWANA. (LAW. 19:16-18 SUV).


Ona maandiko yalivyo wazi.
Anatuambia tusiende huko na huko katikati ya watu wa Mungu kama wachongezi wala tusisimame kinyume na damu ya jirani zetu.
Tusiwamalizie watu ambao tayari wanatokwa damu kwa sababu ya makosa ambayo wameyafanya.
Tusimchukie jirani bali tumkemee ili tusije tukabeba dhambi kwa ajili yao lakini huko kukemea kusifanyikie hadharani na tusifanye kama kisasi au kwa kinyongo dhidi ya mwenzako.
Nimalizie kwa andiko ambalo linatusaidia kuelewa nini maana ya kufunika dhambi au kusitiri makosa.
Sio kuipotezea bali hasa namna tunavyoshughulika nayo.
Ndugu zangu, ikiwa mtu wa kwenu amepotelea mbali na kweli, na mtu mwingine akamrejeza; jueni ya kuwa yeye amrejezaye mwenye dhambi hata atoke katika njia ya upotevu, ataokoa roho na mauti, na kufunika wingi wa dhambi. (YAK. 5:19-20 SUV).
Ameiweka wazi sana kuwa miongoni mwetu mtu akiwa amepotelea mbali na kweli yaani anafanya vitu kinyume na Kweli mtu mwingine amrejeze, sio ndo tunamsukumia mbali kabisa kwa namna tunavyo ihandle situation yake.
Tunapomrejeza mkosaji au mwenye dhambi hata atoke katika njia yake ya upotevu tutakua tunaiokoa roho na mauti na kufunika uwingi wa dhambi.
Kwa hiyo kama unachofanya hakimrejezi huyo mtu uwe na uhakika unachofanya kinamwua huyo mtu na ndo maana nikatangulia kusema jeshi la pekee linaloua majeruhi wake ni Kanisa la Yesu.
Mbaya zaidi ni pale tunapoona tupo sawa katika tunachofanya kwa kunukuu maandiko nje ya muktadha.
Kinachoathiri Kanisa sio makosa yanayofanywa bali namna tunavyoshughulika na hayo makosa yaliyofanywa.
Yesu alisema amri mpya anatuachia.
Tupendane sisi kwa sisi kama Yeye alivyotupenda.
Je tunapokosea Yeye huwa anatuanika?
Anaweza kufanya hivyo mjue!
Anasema tukipendana kama alivyotupenda watu wote watajua kuwa sisi ni wanafunzi Wake.
Ndo maana wanashindea kujua kama sisi ni wanafunzi Wake kwa sababu tunachukiana sana na kuwekeana visasi balaa.
EE MWENYEZI MUNGU TUREHEMU.

Comments

Post a Comment